Saturday, November 17, 2012

RADIO JAMII LOLIONDO YAZINDULIWA

Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia Profesa Makame Mbarawa (aliyeshika mkasi) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kituo cha redio jamii Loliondo katika kijiji cha Ololosokwan - Loliondo Arusha. Kushoto ni mkurugenzi wa UNESCO bibi Vibeke Jensen na kulia ni mkurugenzi wa mawasiliano wa Airtel bi Beatrice Singano. Redio jamii Loliondo imeanzishwa kwa ushirikiano wa shirika la UNESCO, OXFAM na Airtel.

Pichani ni jiwe la msingi linavyonekana baada ya kuzinduliwa kwa redio jamii Loliondo na waziri wa mawasiliano sayansi na teknolojia Profesa Makame Mbarawa katika kijiji cha Ololosokwan, Loliondo Arusha.

Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia Profesa Makame Mbarawa, akiwa katika studio ya redio jamii Loliondo akitangaza kama ishara ya uzinduzi wa redio hiyo.

Picha ya pamoja ya wadau wa redio jamii Liloliondo. Waliokaa kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa halmashauri, Mkurugenzi wa halmashauri Dr. Kuney, Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia Prof. Makame Mbarawa na Mkurugenzi mtendaji wa UNESCO nchini Bibi Vibeke Jensen. Waliosimama kutoka kulia ni Al Amin Yusuph kutoka UNESCO, Mkurugenzi wa shirika la Ilkiramat Foundation na redio jamii Loliondo Yanick Ndoinyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel bi  Beatrice Singano na mdau mwingine wakiwa wamepozi kwenye picha ya pamoja.

**** **** **** **** **** ****
Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia Profesa Makame Mbarawa, ameipongeza kampuni ya mawasiliano nchini ya Airtel na shirika la UNESCO kwa jitihada zao walizozifanya za kuendeleza mawasiliano hasa vijijini.

Prof. Mbarawa ametoa pongezi hizo wakati akiongea na wananchi wa kijiji cha Ololosokwani kilichopo Loliondo Mkoani Arusha wakati wa uzinduzi wa kituo cha redio jamii cha Loliondo.

Akiongea wakati wa uzinduzi huo Prof. Makame Mbarawa amesema amefurahishwa na wadau hao kwa namna wanavyojiunga na jamii kwa kuwaunganisha na sehemu nyingine za dunia kwa kuweka redio jamii Loliondo katika eneo hilo la Ololosokwan, ili nao waweze kupata habari na taarifa muhimu kwa maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa mawasiliano wa Airtel bi Beatrice Singano, amesema Airtel inajisikia furaha kuwa sehemu ya kuchangia maendeleo ya jamii nchini ikiamini kuwa jamii ya kifugaji ya kimaasai inayoishi Ololosokwan kupitia redio hiyo ya jamii na mtandao wa Airtel itabadilika kiuchumi na kimaendeleo kwa kasi katika nyanja zote.

Naye mwakilishi wa UNESCO nchini Al Amin Yusuph, amesema kuwepo kwa redio jamii Loliondo katika eneo la Ololosokwan kutaunganisha wakazi wa eneo hilo na maeneo mengine jirani na mbali na mradi huo wa redio pia UNESCO imeanzisha miradi mingine katika eneo hilo ukiwemo mradi wa Solar ambao utawezesha kina mama kupata kipato kwa kuchajisha simu na kufanya shughuli nyingine zinazohitaji umeme kwa gharama nafuu.

Uanzishwaji wa redio jamii Loliondo utasaidia upatikanaji wa taarifa za habari na mambo muhimu ya kimaendeleo kwa wananchi wa Loliondo ambao kwa muda mrefu walikuwa wakizipata redio za nchi jirani ya Kenya na chache zilizopo nchini kwa masafa ya AM.

No comments:

Post a Comment