Michezo na Burudani


LIGI KUU YA VODACOM TANZANIA BARA KUANZA KUTIMUA VUMBI LEO KATIKA VIWANJA SABA TOFAUTI HAPA NCHINI

Leo ndiyo leo, ambapo timu 14 zinazoshiriki michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom kuwania ubingwa wa Tanzania Bara 2012/2013, zinajitupa uwanjani kwenye viwanja  saba tofauti hapa nchini. 

Mabingwa watetezi wa Ligi hiyo Timu ya Simba Sports Club inajitupa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam kumenyana na African Lyon.

Wana wa Jangwani Timu ya Dar Young African yenyewe itakuwa mgeni wa Tanzania Prisons ya Mbeya ambayo imerejea katika Ligi kuu ya Vodacom Msimu huu, mpira utakaochezwa kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine mjini Mbeya.

Huko Morogoro Polisi Dodoma itakutana na Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa Jamhuri, wakati jijini Mwanza katika uwanja wa CCM Kirumba kutakuwa na mechi kati ya Toto Africans dhidi ya Oljoro JKT.

Nako jijini Tanga Mgambo JKT ambayo imepanda daraja msimu huu, itakutana na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini humo.

Mechi kati ya Azam FC na Kagera Sugar itachezwa kwenye uwanja wa Kaitaba, wakati JKT Ruvu na Ruvu Shooting zitaumana kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es salaam.

Mechi zote zitaanza kuchezwa majira ya saa 10:30 jioni.

Viingilio katika Mechi ya Simba na African Lyon ni kama ifuatavyo; Jukwaa la viti vya rangi ya kijani na bluu ni sh. 5,000 viti vya rangi ya chungwa ni sh. 8,000 huku VIP B na C vitakuwa sh. 15,000 na VIP A ni sh. 20,000.
Viingilio kwa mechi nyingine vitakuwa ni kati ya sh. 3,000 na sh. 10,000

No comments:

Post a Comment