Monday, September 17, 2012

WIKI YA NENDA KWA USALAMA BARABARANI


Wiki ya nenda kwa usalama barabarani kitaifa imefunguliwa leo katika viwanja vya Samora mkoani Iringa.
Mgeni rasmi katika ufunguzi wa wiki hii ya nenda kwa usalama barabarani anatarajiwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Mheshimiwa Dokta Emmanuel Nchimbi ambaye atamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh, Jakaya Mrisho Kikwete.
Wiki ya Nenda kwa usalama barabarani inatarajiwa kufikia kilele chake September 22 mwaka huu, ambapo Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel kwa kuendeleza dhamira yake ya kushirikiana na Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama barabarani katika kuhakikisha ajali za barabarani zinadhibitiwa na kupungua, imeunga mkono kampeni hii.
Kwa miaka minne mfululizo Airtel imekuwa mdhamini wa kampeni hii ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani ambapo mwaka huu mbali na kuchapisha Stickers, imejitolea fulana mia 8 zenye ujumbe maalumu kwa mwaka huu usemao "Pambana na ajali za barabarani kwa vitendo, zingatia sheria".
Makabidhiano ya Fulana hizo yamefanywa na Ofisa Uhusiano wa Airtel Jane Matinde katika ofisi za makao makuu ya polisi usalama barabarani jijini Dar es salaam.
Akizungumza wakati wa hafla maalum ya makabidhiano hayo bi Jane Matinde amesema Airtel imeona ni haki na nisawa kuendelea kuthamini Usalama barabarani na kwamba wana dhamira thabiti ya kuhakikisha Airtel inaelimisha na kuhamasisha jamii na waendesha vyombo vya moto kuzingatia na kutii sheria za Usalama barabarani.
Bi Matinde ameongeza kuwa Airtel Tanzania imeamua kuunga mkono kampeni hii ya nenda kwa Usalama barabarani kwa sababu ongezeko la ajali za barabarani zinaathiri wananchi ambao pia ndio wateja wao wakubwa na kuwaomba watanzania wote kuunga mkono jitihada hizi ili kuhakikisha kwamba vyombo vya moto vinakaguliwa na kubandikwa stika maalum za nenda kwa Usalama barabarani.
Kwa upande wake Kamanda Mkuu wa Usalama Barabarani Mohamedi Mpinga ameishukuru Airtel kwa ushirikiano wao katika mkakati wao wa kupunguza ajali za barabarani, na kutoa hamasa kwa wananchi kujitokeza katika vituo vyote vilivyopo nchini ili magari yao yaweze kukaguliwa na kupata stika za Usalama barabarani.

Afisa Uhusiano wa Airtel Jane Matinde (katikati) akikabidhi Tshirt kwa Kamanda mkuu wa kikosi cha Usalama barabarani Mohamed Mpinga (Kushoto), zilizobeba ujumbe unaosema "Pambana na ajali za barabarani kwa vitendo, zingatia sheria", zitakazotumika katika maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani ambapo kitaifa yanafanyika mkoani Iringa.







No comments:

Post a Comment