Friday, November 06, 2015

HESLB YAJIVUA LAWAMA WANAFUNZI WA VYUO VIKUU KUKOSA MIKOPO 2015/2016


New-Picture-4.jpg

Zaidi ya wanafundi 50,000 watashindwa kuendelea na masomo ya elimu ya juu kutokana na kushindwa kupata mikopo kutoka katika Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB).
Hayo yamebainika ikiwa ni siku nne tangu HESLB kutoa majina ya wanafunzi waliofanikiwa kupata mikopo kwa mwaka wa masomo 2015/2016, huku idadi kubwa ikiwa haimo katika majina hayo.
Katika mwaka huu wa masomo bodi ya mikopo imeweza kuwapatia mikopo wanafunzi 12,000 pekee sawa na 17.1% ya waombaji zaidi ya 70,000, hivyo kufanya idadi ya wanafunzi waliokosa mikopo kufikia asilimia 82.9 ya waombaji wote.
Wanafunzi waliokosa mikopo ya kuwawezesha kujiunga na elimu ya juu na hivyo wazazi wao kutakiwa kugharamia elimu hiyo wameelezea kusikitishwa na hali hiyo huku wakiitaka serikali kuwaangalia kwa jicho la kipekee kwani hawana uwezo wa kuanza masomo pasipo kufadhiliwa na serikali.
Wanafunzi hao walionekana kukata tamaa ya kutimiza ndoto yao ya kujiunga na elimu ya chuo kikuu, wamefika makao makuu ya bodi hiyo huku wakiongozana na baadhi ya viongozi wa serikali ya wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kutaka kujua hatima yao.
“Nimetokea Tabora, wazazi wangu walinipa Sh. 100,000 ya kutumia wakiamini tunapewa mikopo na serikali, lakini tumenyimwa na hatujui hatima yetu, nimebakiwa na Sh. 6,000, naomba serikali ituhurumie, isikie kilio chetu hatustahili kuteseka hivi,” ameeleza Abdul Omary mwanafunzi mteule UDSM.
Fatuma Bakari, mwanafunzi mwingine kutoka UDSM, amesema: “Siwezi kujiunga na Chuo bila mkopo, tumefika hapa ili kuomba bodi ya mikopo itusaidie hatuna tumaini lolote zaidi ya kuomba Mungu atusaidie tuweze kupata mikopo na kuanza masomo.”
Waziri wa Mikopo serikali ya wanafunzi (Daruso), Shitindi Venance ameeleza kutokukubaliana na majibu waliyopewa na uongozi wa juu wa bodi ya mikopo kwani yanakatisha tamaa na kuzima ndoto za wanafunzi wa masikini kusoma chuo kikuu.
“Hapa UDSM ni wanafunzi 600 tu waliopata mikopo kati ya wanafunzi 7,000 waliopangiwa kuanza masomo, hili ni janga kubwa kwa watoto wa masikini kwani hawawezi kujisajili chuoni wala kupata makazi katika mabweni mpaka walipe ada na wengi wametoka mikoani.
“Tunachukua hatua moja mbele na kuamua kulifuatilia suala hili kwa katibu mkuu wa wizara ya elimu na katibu mkuu wa wizara ya fedha kwa sababu bodi bado wanasisitiza tuwe na subira ilihali muda umeenda na wanafunzi wanateseka” ameeleza Shitindi.
Mkurugenzi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Omega Ngole amewaambia wanahabari waliofika ofisini kwake kuwa bodi haistahili kulaumiwa kwani serikali kupitia wizara ya fedha na wizara ya elimu ndio yenye uwezo wa kutenga kiasi cha fedha kulingana na mahitaji ya wakati husika.



Wednesday, November 04, 2015

TAMASHA LA KUSAIDIA WATOTO NJITI NCHINI, KUFANYIKA NOV. 8 LEADERS CLUB


Katika kuadhimisha siku ya  watoto njiti duniani, Taasisi ya Doris Mollel Foundation (DMF) imeandaa tamasha la kwanza  na la aina yake kufanyika nchini siku ya Jumapili Novemba 8. 2015 kwenye viwanja vya Leaders Club, Kinondoni kuanzia majira ya asubuhi mpaka saa 12 jioni huku wasanii mbalimbali wakitarajiwa kushiriki kwa ajili ya kuchangisha fedha za kununulia vifaa vya kusaidia watoto wanaozaliwa na uzito pungufu ama watoto njiti.
Akielezea mbele ya wanahabari jijini Dar es Salaam mapema jana, dhumuni la tamasha hilo ni kuwaleta watanzania pamoja kupata uelewa na mwamko katika kuadhimisha siku hiyo muhimu kwa afya na ustakabali wa mtoto njiti ambapo kulingana na takwimu za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, takribani watoto 88,128 walizaliwa njiti au wakiwa na uzito mdogo nchini kwa kipindi cha mwaka 2014/2015 pekee.
DSC_0027.jpg
Mwenyekiti wa Mfuko wa Doris Mollel Foundation, Bi. Doris Mollel akiwakaribisha wageni mbalimbali na wanahabari wakati wa utambulisho maalum juu ya tamasha linalotarajiwa kufanyika siku ya Jumapili Novemba 8, katika viwanja vya Leaders Club, jijini Dar es Salaam. Kushoto kwake ni  Kaimu Mkurugenzi Mkuu Idara ya Afya, uzazi na watoto,  Bi. Georgina Msemo na kulia kwake ni Dk. Sonal Peter  ambaye ni daktari wa watoto (Pediatrician) kutoka Hospitali ya Agha Khan.

“Lengo ni kuhakikisha kupitia Mfuko huu unasaidia watoto njiti hasa kwa vifaa vya kuwawezesha kusaidia maisha yao. Tunataka kufikisha vifaa 10 kwa kila Kanda chache za awali. Karibuni sana watanzania kwa siku ya Jumapili Novemba 8. Kwa kiingilio cha sh 2,000  pekee kama mchango ambapo utapata burudani ya kipekee kutoka kwa wasanii mbalimbali wakiwemo Barnaba Classic, Mwasiti, kundi la The Voice, Miriam, Baraka De Prince, Ruby, Shilole na wengine wengi.” Amebainisha Doris Mollel.
Aidha, Doris amebainisha kuwa, Watanzania watapata fursa maalum ya kuusikia  wimbo ulioimbwa na baadhi ya wasanii hao watakaoshiriki katika tamasha hilo.
DMF imeongeza kuwa,  baada ya tamasha hilo, kwa kushirikiana na wadhamini pia itatoa vifaa mbalimbali ikiwemo (Suction machines, Oxygen Concentrators na Feeding tubes) hii ni kwa Hospitali za Mikoa nchini ilikuweza kusaidia watoto hao na vifaa hivyo vinatarajiwa kutolewa katika siku ya kilele cha maadhimisho ya mtoto njiti Duniani huku kwa Tanzania ikitarajiwa kufanyika Mkoani Mbeya.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu Idara ya Afya, Uzazi na Watoto,  Bi. Georgina Msemo kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa wizara hiyo amezitaka jamii nchini kujitokeza kwa wingi kusaidia wamama wajawazito wakati wa kipindi chote cha ujauzito kwani kusaidia huko kutapunguza watoto wanaozaliwa kabla ya wakati ama njiti.
“Jamii iwe na huruma kwa wamama wajawazito. Kwani  haya yote yanatokea kutokana na wamama wengi wanakuwa wanafanya kazi ngumu kutopatiwa huduma muhimu na hata wengine kutokwenda kliniki… hivyo ni  jamii ichukue hatua ya kusaidiana na wajawazito kutatua tatizo hili” alieleza Bi Msemo katika taarifa yake hiyo aliyoitoa wakati wa hafla hiyo ya utambulisho wa tamasha la kuchangia fedha za kusaidia watoto njiti.
DSC_0096.jpg
Wasanii wa kundi la The Voice, Barnaba Classic na wengineo wakiimba kwa hisia wimbo maalum wa kumpa matumaini Mama mjamzito na aliyejifungua mtoto njiti katika kusaidia maisha yake.
DSC_0107.jpg
Bi. Doris Mollel akiwapongeza wasanii hao kwa kumuunga mkono katika tukio hilo likiwemo la kuimba wimbo maalum na pia kutumbuiza siku ya Jumapili Novemba 8.2015.
DSC_0088.jpg
Kundi la The Voice wakiimba wimbo huo ambapo baadhi ya sehemu walizorekodia ni kwenye wodi ya watoto njiti.



NB: Shukran kwa Modewjiblog kwa habari na picha

Saturday, August 08, 2015

TEKNOLOJIA MPYA YA KUOTESHA MAZAO KWA MAJI NA VIRUTUBISHO BILA KUTUMIA UDONGO

HABARI NJEMA KWA MFUGAJI

Katika pitapita zangu kwenye mabanda ya maonyesho ya kilimo nane nane katika viwanja vya TASO Njiro - Arusha, nikakutana na kitu kilichonivutia katika banda la Halmashauri ya wilaya ya Arusha - Arusha DC, nikaona ni vema kama nitaweza kukushirikisha ewe mfugaji wa mifugo ya nyumbani mfano kware, kuku, mbuzi na hata ng'ombe, kutumia teknolojia mpya inayoitwa HYDROPONICS.



HYDROPONICS ni teknolojia ya kuotesha mazao kwa maji na virutubisho bila kutumia udongo.

FAIDA ZAKE: Ni rahisi kutumia teknolojia hii kwani inaweza kufanyika mahali popote. Husaidia kuvuna na kupata  mazao mengi kwa muda mfupi. Haina madhara kwa afya za mifugo na binadamu kma mlimaji alizingatia  maelekezo.

Hutumia kiwango kidogo cha maji na haihitaji udongo, huku ikiokoa matumizi ya ardhi.

HYDROPONICS FODDER - ni kimea kinachooteshwa kwa kutumia mbegu za shayiri ili kupata chakula cha mifugo mfano kuku, ng'ombe, sungura, nguruwe, mbuzi, kondoo n.k.



Ili kuotesha mbegu zako kwa utaratibu huu utahitaji kuwa na banda maalum kwa kuoteshea lenye ukubwa wowote, trei za plastic au aluminium zenye matundu (kama ni aluminium hakikisha sio material yale yanayopata kutu pindi yakiingia maji).

Pia utahitaji kuwa na virutubisho vya hydroponics (Hydroponics Nutrients), Sprayer (Chupa ya kunyunyiza maji yenye matundu madogo ili maji yamwagike kama mvua), Mbegu za Shayiri au ngano (chagua mbegu ambazo hazijashambuliwa na wadudu), na pia unatakiwa uwe na chombo cha kuloweka mbegu na hapa waweza kutumia ndoo ya aina yoyote, kwani itatakiwa uziloweke kwa siku chache.

Kwa  maelezo ya kitaalamu zaidi wasiliana  na  namba hii 0766 503 330