Wednesday, November 04, 2015

TAMASHA LA KUSAIDIA WATOTO NJITI NCHINI, KUFANYIKA NOV. 8 LEADERS CLUB


Katika kuadhimisha siku ya  watoto njiti duniani, Taasisi ya Doris Mollel Foundation (DMF) imeandaa tamasha la kwanza  na la aina yake kufanyika nchini siku ya Jumapili Novemba 8. 2015 kwenye viwanja vya Leaders Club, Kinondoni kuanzia majira ya asubuhi mpaka saa 12 jioni huku wasanii mbalimbali wakitarajiwa kushiriki kwa ajili ya kuchangisha fedha za kununulia vifaa vya kusaidia watoto wanaozaliwa na uzito pungufu ama watoto njiti.
Akielezea mbele ya wanahabari jijini Dar es Salaam mapema jana, dhumuni la tamasha hilo ni kuwaleta watanzania pamoja kupata uelewa na mwamko katika kuadhimisha siku hiyo muhimu kwa afya na ustakabali wa mtoto njiti ambapo kulingana na takwimu za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, takribani watoto 88,128 walizaliwa njiti au wakiwa na uzito mdogo nchini kwa kipindi cha mwaka 2014/2015 pekee.
DSC_0027.jpg
Mwenyekiti wa Mfuko wa Doris Mollel Foundation, Bi. Doris Mollel akiwakaribisha wageni mbalimbali na wanahabari wakati wa utambulisho maalum juu ya tamasha linalotarajiwa kufanyika siku ya Jumapili Novemba 8, katika viwanja vya Leaders Club, jijini Dar es Salaam. Kushoto kwake ni  Kaimu Mkurugenzi Mkuu Idara ya Afya, uzazi na watoto,  Bi. Georgina Msemo na kulia kwake ni Dk. Sonal Peter  ambaye ni daktari wa watoto (Pediatrician) kutoka Hospitali ya Agha Khan.

“Lengo ni kuhakikisha kupitia Mfuko huu unasaidia watoto njiti hasa kwa vifaa vya kuwawezesha kusaidia maisha yao. Tunataka kufikisha vifaa 10 kwa kila Kanda chache za awali. Karibuni sana watanzania kwa siku ya Jumapili Novemba 8. Kwa kiingilio cha sh 2,000  pekee kama mchango ambapo utapata burudani ya kipekee kutoka kwa wasanii mbalimbali wakiwemo Barnaba Classic, Mwasiti, kundi la The Voice, Miriam, Baraka De Prince, Ruby, Shilole na wengine wengi.” Amebainisha Doris Mollel.
Aidha, Doris amebainisha kuwa, Watanzania watapata fursa maalum ya kuusikia  wimbo ulioimbwa na baadhi ya wasanii hao watakaoshiriki katika tamasha hilo.
DMF imeongeza kuwa,  baada ya tamasha hilo, kwa kushirikiana na wadhamini pia itatoa vifaa mbalimbali ikiwemo (Suction machines, Oxygen Concentrators na Feeding tubes) hii ni kwa Hospitali za Mikoa nchini ilikuweza kusaidia watoto hao na vifaa hivyo vinatarajiwa kutolewa katika siku ya kilele cha maadhimisho ya mtoto njiti Duniani huku kwa Tanzania ikitarajiwa kufanyika Mkoani Mbeya.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu Idara ya Afya, Uzazi na Watoto,  Bi. Georgina Msemo kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa wizara hiyo amezitaka jamii nchini kujitokeza kwa wingi kusaidia wamama wajawazito wakati wa kipindi chote cha ujauzito kwani kusaidia huko kutapunguza watoto wanaozaliwa kabla ya wakati ama njiti.
“Jamii iwe na huruma kwa wamama wajawazito. Kwani  haya yote yanatokea kutokana na wamama wengi wanakuwa wanafanya kazi ngumu kutopatiwa huduma muhimu na hata wengine kutokwenda kliniki… hivyo ni  jamii ichukue hatua ya kusaidiana na wajawazito kutatua tatizo hili” alieleza Bi Msemo katika taarifa yake hiyo aliyoitoa wakati wa hafla hiyo ya utambulisho wa tamasha la kuchangia fedha za kusaidia watoto njiti.
DSC_0096.jpg
Wasanii wa kundi la The Voice, Barnaba Classic na wengineo wakiimba kwa hisia wimbo maalum wa kumpa matumaini Mama mjamzito na aliyejifungua mtoto njiti katika kusaidia maisha yake.
DSC_0107.jpg
Bi. Doris Mollel akiwapongeza wasanii hao kwa kumuunga mkono katika tukio hilo likiwemo la kuimba wimbo maalum na pia kutumbuiza siku ya Jumapili Novemba 8.2015.
DSC_0088.jpg
Kundi la The Voice wakiimba wimbo huo ambapo baadhi ya sehemu walizorekodia ni kwenye wodi ya watoto njiti.



NB: Shukran kwa Modewjiblog kwa habari na picha

No comments:

Post a Comment